Home » Bez kategorii » Wakala wa Mafunzo ya Mifugo Tengeru – Mshiriki wetu katika Mradi wa Misaada ya Kipolishi 2019/2020.

Wakala wa Mafunzo ya Mifugo Tengeru – Mshiriki wetu katika Mradi wa Misaada ya Kipolishi 2019/2020.

LITA, Kampasi ya Tengeru iko kwenye uwanda wa chini wa Mlima Meru, kilomita 14 kutoka jiji la Arusha. Kwa ujumla, hali ya hewa ni bora kwa masomo na shughuli za kilimo na ufugaji. Kampasi hii ni mojawapo ya Kampasi nane za Wakala chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Ilianzishwa mnamo mwaka 1952 baada ya kuondoka kwa wakimbizi wa Kipolishi mwishoni mwa Vita vya pili vya dunia. Kampasi hii inayo historia muhimu kwa kuwa Makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka 1967 hadi 1977. Katika kipindi hiki Kampasi ilikuwa bado inaendesha mafunzo ya astashahada katika uzalishaji na uchakataji wa maziwa. Baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mnamo mwaka 1977. Kampasi ilianza tena shughuli zake za mafunzo kwa kutoa astashahada, stashahada na kozi fupi kwa wakulima na wafugaji. Kutokana na ubora wa hali ya juu wa mafunzo inayotoa, Kampasi ilipokea hati kamili ya usajili na ithibati kutoka Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE). Hivi sasa, Kampasi inatoa; astashahada ya Afya ya Wanyama na Uzalishaji (Kiwango cha 4 cha Nationa Technical Award (NTA), astashahada ya Afya na Uzalishaji wa wanyama (kiwango cha 5 cha NTA) na Stashahada ya kawaida katika Afya na Uzalishaji wa wanyama (kiwango cha 6 cha NTA) na kozi fupi kwa kadiri ya mahitaji ya wadau.Hivi sasa, Kampasi hii ina wafanyakazi wa kudumu 42; kati yao 35 ni wakufunzi na 07 ni wafanyakazi wasaidizi. Katika mwaka wa masomo (2018/19) kampasi ilidahili wanafunzi 760 (kwa kozi zote ndefu na fupi) na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi 1700 katika mwaka wa masomo 2021/2022 baada ya uboreshaji wa miundombinu wezeshi kama vile mabweni, maabara, madarasa nk.